Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nandagala, Mhe. Andrew Chikongwe, ameeleza kuwa mbio za Nandagala Marathon zimeweka historia kwa kuwa ni za kwanza kufanyika katika ngazi ya kata katika Wilaya Ruangwa.
Akizungumza leo Septemba 28, 2024, katika viwanja vya Stendi Nandagala, Mhe. Chikongwe amesema,
"Kwa kawaida, Marathon hizi hufanyika katika ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa, lakini kwa ngazi ya Kata, hii ni ya kwanza kufanyika wilayani Ruangwa na kanda yote ya Kusini." Ameongeza kuwa tukio hilo limeonesha mwelekeo mpya katika kukuza michezo na kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki shughuli za maendeleo.
Mbio hizo zimehusisha washiriki kutoka Wilaya za Ruangwa, Nachingwea, na Liwale, ambapo waneshindana katika mbio za kilomita 21, kilomita 10, kilomita 5, na kilomita 3 kwa wanafunzi wa shule za msingi, Washindi wa kila kundi wamejinyakulia zawadi nono, hali iliyoongeza msisimko na hamasa miongoni mwa washiriki na watazamaji.
Aidha, Mhe. Chikongwe ametumia fursa hiyo kuipongeza Redio Jamii ya Ruangwa, Ruangwa FM, kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha mbio hizo. "Nawashukuru sana Ruangwa FM, wamejitoa kwa nguvu zao zote kuhakikisha Nandagala Marathon inafanikiwa, bila shaka wamefanya kazi kubwa ya kulipa hadhi tukio hili," amesema Mhe. Chikongwe
Sambamba na pongezi hizo, Mhe. Chikongwe pia ametoa wito kwa wadau mbalimbali na wananchi kuendelea kushirikiana katika shughuli za maendeleo, siyo tu ngazi ya kata bali pia Wilaya na Mkoa kwa ujumla, amesema mshikamano huu unapaswa kuendelezwa katika sekta nyingine ili kuleta ustawi wa jamii.
NANDAGALA MARATHON:
HALI YA ZAMANI, SASA NA MUSTAKABALI.
Zamani, matukio makubwa ya michezo kama marathon yalikuwa nadra kufanyika ngazi ya kata wilayani Ruangwa, hali iliyosababisha wananchi wengi kukosa fursa ya kushiriki kwenye mashindano hayo. Hata hivyo, tukio hili la kwanza katika Kata ya Nandagala linaashiria mwanzo mpya, ambapo michezo inaweza kuwa kiungo muhimu cha umoja na maendeleo katika jamii.
Kwa sasa, mbio hizi zimeonyesha kuwa michezo inaweza kuhamasisha ushiriki mkubwa wa wananchi, si tu kama washiriki bali pia wadau wa maendeleo. Washindi wa mbio hizi, pamoja na kupata zawadi, wameonesha mfano wa kuigwa kwa kujitoa na kuchangia maendeleo ya kijamii kupitia michezo.
Kwa siku zijazo, kuna haja ya kuimarisha ushirikiano baina ya wadau mbalimbali ili kuhakikisha mbio kama hizi zinafanyika mara kwa mara, si tu katika kata bali pia katika Vijiji na Wilaya nzima kwa ujumla. Hii itasaidia kuongeza kasi ya maendeleo ya michezo na kuleta fursa mpya kwa vijana na jamii kwa ujumla. Serikali na sekta binafsi zinapaswa kuendelea kutoa msaada wa vifaa, rasilimali, na motisha kwa washiriki na waandaaji wa matukio kama haya.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa