Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania Mhe. Dunstan Kitandula, amefanya kikao na wananchi wa kijiji cha Mbangala kilichopo Kata ya Makanjiro wilayani Ruangwa.
Kikao hicho kimefanyika leo Julai 17, 2024 kikiwa na lengo la kusikiliza kero, changamoto, na kutoa elimu juu ya athari zinazosababishwa na wanyama pori, hususani Tembo, katika kijiji hicho.
Aidha Mhe. Kitandula amewashukuru wananchi wa Mbangala kwa uwazi wao katika kueleza matatizo wanayokabiliana nayo na amewahakikishia kwamba Serikali ipo bega kwa bega na wananchi katika kutatua changamoto hiyo. Amesisitiza uvumilivu kutoka kwa wananchi kwani Serikali iko kazini kutafuta suluhisho la kudumu.
Katika hatua nyingine Mhe. Kitandula ameleza kwamba Serikali imejipanga kununua helikopta mbili zitakazotumika katika zoezi la kuondoa Tembo karibu na makazi ya watu.
Sambamba na hayo, Mhe. Kitandula amesema kuwa Serikali imepokea maombi 377 ya kifuta machozi kutoka kwa wananchi waliokumbwa na matatizo ya Tembo kutoka Wilaya ya Ruangwa na imeahidi kuyashughulikia haraka na kuhakikisha wale wanaostahili wanalipwa fidia zao.
“Ninapata machungu kama mnayopata ninyi maana naelewa nini mnapitia kwa wakati huu, Serikali itashughulikia kero zote na ni suala la muda tu, pia mnatakiwa kufahamu kwamba shughuli za binadamu zimefika mpaka kwenye maeneo ya hifadhi za wanyama na kuwafanya wanyama kutoka kwenye makazi yao. Mfano, zamani Tanzania ilikuwa na Tembo 300,000 lakini hakukuwa na vurugu kama hizi za sasa ambapo tuna tembo 60,000 na tatizo limekuwa kubwa sana” amesema Mhe. Kitandula.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Hassan Ngoma, ameishukuru Serikali kwa msaada na jitihada za kudhibiti tatizo la Tembo katika kijiji cha Mbangala.
“Serikali inafanya kazi nzuri sana kila tukihitaji msaada wataalamu wanafika mapema sana na kutusaidia, kipekee nikushukuru Mhe. Naibu Waziri kwa ujio wako najua utatusaidia kupata majawabu ya wanambangala" amesema Mhe. Ngoma.
Nao, wananchi wa Kijiji cha Mbangala wametoa maoni, kero na mapendekezo yao kwa Serikali, wakieleza kuwa Tembo wanaleta umasikini kwa kuharibu mashamba yao na kuiomba Serikali kuchukua hatua zaidi kudhibiti tatizo hilo.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa