Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Andrew Chikongwe, ametoa rai kwa wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa na wanapewa elimu bora pamoja na matunzo wanayostahili, hayo yamesemwa jana, Oktoba 30, 2024, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambapo wilayani Ruangwa yamefanyika kata ya Nandagala.
Mhe. Chikongwe, ambaye amekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, ametoa rai kwa wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa na wanapewa elimu bora pamoja na matunzo wanayostahili.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mazingira salama kwa watoto wa kike ili waweze kukua na kutimiza ndoto zao.
“Katika dunia ya sasa kuna watu wema lakini pia wapo wabaya wanaoweza kuharibu maisha ya watoto wetu,” amesema Chikongwe, akihimiza wazazi kuwapa watoto nafasi ya kuzungumza kwa uwazi bila woga.
Sambamba na hayo, amewahimiza walimu kuendelea kuwalea watoto katika maadili mema na kuwa na mtazamo chanya kuhusu maisha.
“Walimu tunawaomba muendelee kutulelea watoto wetu kwenye maadili mwema,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Child Welfare ameushukuru uongozi wa Wilaya ya Ruangwa kwa ushirikiano na mapokezi mazuri waliouonyesha katika kufanikisha maadhimisho hayo.
Maadhimisho hayo yamelenga kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kulinda haki za mtoto wa kike na kumwezesha kupata fursa sawa na kujijengea mustakabali bora. Siku hiyo pia imetumika kuwaelimisha wazazi na walezi kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki ya elimu, ulinzi, na malezi bora. Viongozi na wadau wametoa shukrani kwa juhudi za wilaya hiyo kuendeleza ustawi wa watoto wa kike na kuihimiza jamii kushirikiana katika kujenga msingi imara kwa kizazi kijacho.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa