Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Mhe. Andrew Chikongwe, ametoa wito kwa wajasiriamali wa Wilaya hiyo kuongeza juhudi katika kukuza biashara zao. Akizungumza leo, tarehe 6 Agosti 2024, alipotembelea banda la Wilaya ya Ruangwa katika maonesho ya Nanenane kanda ya kusini yanayofanyika katika viwanja vya Ngongo- Lindi Manispaa na kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wajasiriamali hao.
Mhe. Chikongwe amesisitiza umuhimu wa kujitangaza kupitia njia mbalimbali, ikiwemo Radio Ruangwa FM, ili kufikia wateja wengi zaidi. Amesema kuwa kujitangaza ni njia moja ya kuongeza mauzo na kupata fursa za kupata mikopo, hivyo kuwawezesha wajasiriamali kufanya mambo makubwa zaidi katika biashara zao.
Aidha, ametoa mfano wa mafanikio yake binafsi, Chikongwe ameeleza kuwa yeye ni msindikaji wa bidhaa za vitafunwa kama mikate, donati, mandazi, na sikonzi. Amefafanua kuwa ameweza kukuza biashara yake kwa kutumia mbinu mbalimbali za kujitangaza katika maeneo tofauti.
Sambamba na hayo, amepongeza kwa maandalizi mazuri na makubwa.
“mara ya kwanza Halmashauri yetu tumefanya vizuri sana kwenye vipando vya mazao na vipando vya malisho ya Mifugo nawapongeza sana kwa kazi nzuri niwaombe muendelee kuchapa kazi” amesema Mhe. Chikongwe.
Ikumbukwe, maonesho ya Nanenane ni fursa muhimu kwa wajasiriamali wa Ruangwa na maeneo mengine kushiriki na kuonyesha bidhaa zao. Huu ni wakati wa kujifunza mbinu mpya za kukuza biashara, kupata masoko mapya, na kujitangaza kwa wateja wapya. Nanenane inaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wajasiriamali kuimarisha mitandao yao na kuongeza tija katika biashara zao.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa