Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mhe. Andrew Chikongwe, amewahimiza watendaji wa Kata kuwa mabalozi wa kilimo cha kisasa kwa kuonesha mfano wa vitendo, akizungumza katika semina maalum ya tathmini na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo iliyofanyika leo, Septemba 17, 2024, katika Shule ya Sekondari Ruangwa, Mhe. Chikongwe amewataka watendaji wa Kata kuhakikisha kwamba wanatekeleza kilimo cha kisasa kwa kutumia mbolea bora na mbinu za kisasa, na hivyo kuwa mifano hai kwa wananchi wa Wilaya ya Ruangwa.
Mhe. Chikongwe amesisitiza kuwa Watendaji wanapaswa kuonesha kwa vitendo matumizi ya teknolojia ya kisasa na kutoa mfano wa jinsi ya kupanda mazao bora ili kuvutia na kuhamasisha wananchi. Ameongeza kuwa, watendaji wakishiriki moja kwa moja katika kilimo cha kisasa kutasaidia kuongeza uelewa na kuhamasisha wakulima kuiga mifano yao.
Aidha, Mhe. Chikongwe ameongeza kuwa lengo kuu la juhudi hizi ni kuifanya Wilaya ya Ruangwa kuwa kinara wa kilimo nchini. Watendaji wakiwasaidia wananchi kwa vitendo, wataongeza ufanisi wa kilimo na kuboresha uzalishaji, na hivyo kusaidia Wilaya kuwa kitovu cha utalii na uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Ameongezea kwa kusema “hali ya kilimo katika Wilaya ya Ruangwa imekuwa ya tofauti kutokana na jitihada mpya zinazofanywa na Serikali, ikiwa ni pamoja na kupeleka pembejeo za kutosha maeneo yote, hivyo basi kuna matumaini ya kuona mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo. Wataalamu wa kilimo wanapaswa kuendelea kutoa elimu kwa wakulima na kuwa sehemu ya utekelezaji wa mbinu bora za kilimo ili kuhakikisha kwamba mikakati ya kilimo inatekelezwa kwa ufanisi” amesema Mhe. Chikongwe.
Ikumbukwe, Kwa kuzingatia mifano bora na kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mafunzo sahihi na vifaa vya kisasa, Wilaya ya Ruangwa inaweza kufikia malengo yake ya kuwa kiongozi katika kilimo. Ili kufanikisha hilo, ni muhimu kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wakulima, huku ikifanyika kazi kwa ukaribu na wataalamu wa kilimo na wadau wengine, hii itasaidia kuimarisha kilimo bora na kuhakikisha kuwa Ruangwa inakuwa mfano wa kuigwa katika kilimo cha kisasa nchini.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa