Mratibu wa Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Mkoa wa Lindi 2025 Ndugu Mwinjuma Mohamed Mkungu, ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Lindi, ameeleza kuwa maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa wananchi na wadau wa madini kujifunza, kubadilishana uzoefu, na kuimarisha mahusiano ya kibiashara.
Akizungumza leo 14 Juni, 2025 wakati akitoa taarifa ya uratibu wa zoezi hilo, wakati wa kufunga maonesho hayo amesema kwa siku nne kuanzia Juni 11 hadi 14, maonesho yamehusisha mabanda zaidi ya 120 yakiwasilisha huduma, bidhaa na teknolojia mbalimbali zinazohusiana na sekta ya madini, kati ya hayo mabanda 85 yamekuwa ya wachimbaji na taasisi za umma.
Aidha, ameongeza kuwa maonesho hayo yamekuwa sehemu ya utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu ya Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ya kuufanya Mkoa wa Lindi kuwa kitovu cha uchumi kupitia sekta ya madini.
“Maonesho haya yamekuwa jukwaa la kipekee linalowawezesha wachimbaji na wawekezaji kujifunza na kushirikiana kwa karibu, jambo linalochochea ukuaji wa sekta ya madini hapa Lindi,” amesema Mkungu.
Vilevile, Mkungu ameongeza kuwa mafanikio ya maonesho ya mwaka 2023 yameanza kuonekana kwa kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji, ajira, mapato ya Serikali, na kubadilika kwa maisha ya wananchi wanaojihusisha na sekta hiyo.
Mbali na hayo, amepongeza wadhamini wakuu wa maonesho, wakiwemo Ellianje Genesis, Umoja wa Vikundi vya Wachimbaji Wadogo (UVIWAMA), MAST, Lindi Jumbo, Silverstone Enterprises Ltd, na PMBet, pamoja na taasisi zaidi ya 50 zilizotoa michango yao.
Ikumbukwe, kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu ni “Madini na Uwekezaji, Fursa ya Kiuchumi Lindi. Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025.”
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa