Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, leo Octoba 29, 2024 amezindua rasmi zoezi la uwekaji wa vifaranga vya samaki katika mabwawa yaliyopo Kijiji cha Nahanga, Kata ya Mandawa, wilayani Ruangwa, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika zoezi hilo ambalo jumla ya vifaranga 7,000 vimepandikizwa kwenye mabwawa hayo, ikilinganishwa na lengo lililokusudiwa la kupandikiza vifaranga 6,000, ambapo vifaranga 1,000 vya ziada vimewekwa ili kufidia upotevu unaoweza kutokea.
Mhe. Ngoma amepongeza juhudi za Serikali katika kuanzisha mradi huo muhimu, ambao unalenga kuongeza kipato na fursa za ajira kwa jamii ya Ruangwa, na ameeleza kuwa mradi huo utakuwa kichocheo muhimu cha maendeleo katika sekta ya uvuvi wilayani humo.
Aidha, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndg. Radhidi Namkulala, ameishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo na kuahidi kuhakikisha mradi unalindwa na kuleta matokeo yanayotarajiwa.
“Tunashukuru sana kwa mradi huu wa kimkakati, tutaulinda na kuhakikisha unazaa matunda kama ilivyokusudiwa,” amesema Namkulala.
Naye mwakilishi kutoka Wizara ya Uvuvi, Ndg. John Malya, amesisitiza umuhimu wa kufuata maelekezo ya wizara kwa wanakikundi wanaosimamia mradi huo, akisisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia miongozo yote ili kufanikisha mradi kwa asilimia 100.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Mhe. Andrew Chikongwe, ameipongeza Serikali kwa mradi huo wa ufugaji wa samaki na kusema kuwa ni fursa adhimu kwa wakazi wa Ruangwa kujifunza na kukuza uchumi.
“Mradi huu ni darasa muhimu sana kwa wafugaji wa samaki, tunashukuru sana kwa fursa hii, wanamandawa na wanaruangwa kwa ujumla tuutunze mradi huu wenye uwekezaji wa thamani kubwa sana” amesema Chikongwe.
Naye, Diwani wa Kata ya Mandawa, Mhe. Rashid Lipei, amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kutunza mradi huo na kuhakikisha unakuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Hata hivyo, Wananchi wa Kata ya Mandawa, wakiongozwa na Bi. Asha Issa, wameeleza furaha yao kwa mradi huo, wakisema ni fursa adimu kwao kupata ujuzi na kuboresha maisha yao.
“Mradi huu umetuongezea matumaini na tumefurahia sana, tutaushika vizuri kama tulivyoelekezwa,” amesema Bi. Asha.
Ikumbukwe, mradi huo wa mabwawa ya ufugaji wa samaki ni moja ya uwekezaji wa Serikali unaolenga kuboresha sekta ya uvuvi nchini na kuinua maisha ya wananchi kwa kuwawezesha kujipatia kipato kupitia ufugaji endelevu.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa