Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe.Hassan Ngoma amekuwa mgeni rasmi katika shughuli ya tathimini na kuhitimisha kambi ya madaktari bingwa wabobezi usiku wa kuamkia leo Jumatano Mei 15, 2024 katika ukumbi wa Ruangwa Pride Hotel, na kumuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Faisal Said kusimamia ipasavyo na kuhakikisha dawa zilizotelewa na Amana Bank zinagaiwa bure kabisa kwa wagonjwa na zisiuzwe.
"Amana Bank wametupatia bure, kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji, basi Mganga Mkuu kasimamie kuhakikisha dawa hizo zinatolewa kwa wagonjwa bure isiuzwe hata punje"
Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo Jumatano, Mei 15 2024 katika hafla ya tathimini na kuhitimisha kambi ya Madaktari bingwa wabobezi wa magonjwa ya binadamu iliyofanyika katika ukumbi wa Ruangwa Pride Hotel wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Kambi ya Madaktari bingwa wabobezi wa magonjwa ya binadamu imefanyika kwa siku 3 pekee ikianzia siku ya Jumapili tarehe 12 Mei na kutamatika Jumanne Mei 14, 2024 katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa na takribani wagonjwa 1580 wamepatiwa huduma ikiwa wagonjwa 24 wamefanyiwa huduma ya upasuaji.
Aidha Mhe. Ngoma amewashukuru Madaktari bingwa, Taasisi ya Jamiiyatul Akhlaaqul Islam (JAI) pamoja na Amana Bank kwa huduma waliyoitoa kwa wananchi wa Ruangwa kwani jambo walilolifanya ni kubwa sana la kuokoa uhai wa wananchi tena bila malipo kwani kama wangeamua kutoza pesa wananchi ingewagharimu kutoa pesa nyingi sana kutokana na magonjwa waliyonayo.
Kwa upande wao Madaktari bingwa wakiongozwa na Dkt. Mohamed Mohamed wamemshukuru Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Wilaya, Taasisi ya JAI pamoja na Amana Bank kwa ushirikiano mzuri na ukarimu waliouonesha kwao katika kufanikisha zoezi la matibabu kwa wananchi wa Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa