Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, amefungua rasmi Kikao cha Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Mkoa wa Lindi kilichofanyika leo Aprili 10, 2025 katika Ukumbi wa mikutano wa Ruangwa Pride Hotel, wilayani Ruangwa.
Kikao hicho kimewakutanisha Wakuu wa Shule zote za Sekondari kutoka katika Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Lindi, kikilenga kubadilishana uzoefu, kujadili mafanikio na changamoto, pamoja na kufahamishana taarifa za mapato na matumizi ya shule wanazozisimamia.
Akizungumza mara baada ya kupokea risala ya viongozi wa umoja huo, Mhe. Ngoma amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa walimu katika maendeleo ya elimu, na akaahidi kuwasilisha changamoto walizozitaja kwa viongozi husika ili hatua zichukuliwe kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
“Changamoto zenu nimezisikia na nimezipokea kwa uzito unaostahili. Nitaendelea kuwa kiunganishi kati yenu na viongozi wa ngazi za juu ili kuhakikisha sekta ya elimu mkoani Lindi inaendelea kuimarika,” amesema Mhe. Ngoma.
Kikao hicho pia kimebeba dhamira ya kuimarisha mshikamano baina ya Wakuu wa Shule na kuweka mikakati ya pamoja ya kuinua ufaulu wa wanafunzi katika ngazi ya Sekondari kwa Mkoa wa Lindi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa