Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, leo Septemba 26, 2025 ameshiriki mafunzo ya Extractive Baraza yaliyoandaliwa na taasisi ya HakiRasilimali katika Hotel ya Ruangwa Pride, akisisitiza ushirikishwaji wa jamii na wadau katika sekta ya uchimbaji madini.
Mafunzo hayo yamewaleta pamoja wanajamii, wadau wa maendeleo na viongozi wa eneo hilo ili kujadili fursa na changamoto za sekta ya uchimbaji. Aidha, washiriki wamepata nafasi ya kuangazia namna rasilimali zinavyoweza kutumika kwa faida ya wote, pamoja na mbinu za kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya mapato yatokanayo na uchimbaji.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mhe. Ngoma, amesema ushiriki wake unaashiria dhamira ya Serikali ya kusikiliza wananchi na kushirikiana nao katika kupanga maendeleo.
“Serikali inataka kuona kila mwananchi anapata nafasi ya kushiriki, kutoa maoni na kueleza matarajio yake kuhusu sekta ya uchimbaji, sekta hii ina fursa kubwa na manufaa yake yanapaswa kuwafikia wananchi wote kwa usawa”. amesema Mhe. Ngoma.
Zaidi ya hayo, washiriki wamejadili namna sekta ya uchimbaji inaweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kushirikisha makundi yote, hususan vijana na wanawake. Wameona kuwa ushiriki wa makundi hayo ni msingi wa kuleta ustawi wa jamii kwa usawa na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika maendeleo.
Hata hivyo, baraza limeweka msisitizo katika mshikamano kati ya jamii na wadau kwa kusisitiza kuwa uwazi wa taarifa ni chachu ya kuimarisha imani na ushirikiano. Lakini pia, Washiriki wamekubaliana kuwa utaratibu wa kutoa taarifa wazi kuhusu mapato na matumizi ya sekta ya uchimbaji utasaidia kujenga uwajibikaji wa pamoja na kuimarisha maendeleo ya muda mrefu.
Halikadhalika, changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya uwekezaji wa uchimbaji, ikiwemo athari za kimazingira, ajira na uhusiano wa kijamii, zimejadiliwa kwa kina. Washiriki wamesema kuwa majadiliano ya aina hii ni jukwaa muhimu la kutafuta suluhu za pamoja zinazojenga uelewano kati ya wananchi na wawekezaji.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wengine Mohamedi Chilemba amesema, wanaishikuru taasisi ya Hakirasilimali kwani mafunzo hayo yamewajengea uwelewa mpana kuhusu Sekta ya uchimbaji akisisitiza kwamba mshikamano wa jamii ndio msingi wa maendeleo endelevu.
“Kauli mbiu yetu katika mafunzo haya imebeba maana kubwa tunawashukuru sana wawezeshaji wetu tumejifunza mengi kikubwa siku zote nitaishika kauli mbiu ya mafunzo haya isemayo “A community that speaks together, grows together” ikimaanisha mshirikiano wa jamii ndio njia ya kuleta maendeleo jumuishi na ya kudumu. Amesema” Mohamedi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa