Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Fabian Chonya, amefanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa hosteli za timu ya Namungo FC na kutoa agizo la kuhakikisha kazi hiyo inakamilika mwishoni mwa mwezi Agosti 2025.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi iliyofanyika leo tarehe 31 Julai 2025, Mkurugenzi Chonya ameambatana na Wakuu wa Idara, Vitengo pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri hiyo kwa lengo la kujiridhisha na hatua ya utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya michezo.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi, Mkurugenzi Chonya amesema ni muhimu hosteli hizo zikakamilika kwa wakati ili kuwapa wachezaji wa Namungo FC mazingira bora ya kujiandaa kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC. Amesisitiza kuwa timu hiyo inapaswa kuhamia rasmi katika hosteli hizo mapema mwanzoni mwa msimu wa ligi.
“Tunataka Namungo FC iwe na mazingira bora ya kambi, ili iweze kujiandaa kikamilifu na kufanya vizuri zaidi kwenye ligi, amesema Chonya.
Aidha, ameelekeza wakandarasi kuongeza kasi ya kazi na kuhakikisha viwango vya ubora vinafuatwa, huku akiwataka wasimamizi wa mradi kufuatilia kwa karibu kila hatua ya utekelezaji ili kuepuka ucheleweshaji usio wa lazima.
Zaidi ya hayo, Mkurugenzi ameeleza dhamira ya Serikali ya Wilaya ya Ruangwa ya kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya michezo, hasa kwa timu zinazowakilisha Wilaya katika mashindano ya kitaifa, ili kukuza vipaji na kuinua jina la Ruangwa kimichezo.
Vilevile, viongozi na wataalamu walioambatana naye wameahidi kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kuhakikisha ujenzi wa hosteli hizo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Kwa ujumla, mradi wa hosteli za Namungo FC ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa katika kuimarisha mazingira ya michezo na kuwawezesha wanamichezo wa ndani kupata nafasi ya kushindana katika viwango vya juu.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa