Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack leo, Novemba 06, 2025 ameongoza kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe na Afua za Lishe Mkoa kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Juni 2025 kilichofanyika katika Ukumbi mkubwa wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Telack amewataka viongozi na watendaji wote kuhakikisha wanasimamia ipasavyo utekelezaji wa shughuli za lishe katika maeneo yao sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu lishe bora ili kujenga jamii yenye afya.
“Lishe ni kipaumbele, Lishe ni chakula ni dawa, mwili wako ni kile unachokula. Hakikisheni fedha za lishe zinatoka kwa wakati na zinatumika kama ilivyokusudiwa. Kina baba na mama wajawazito wahimizwe kwenda kliniki pamoja ili kubaini mapema changamoto za upungufu wa damu na lishe na waweze kupata njia za kukabiliana nazo kwa pamoja ili kuimarisha afya ya mama kipindi cha ujauzito na mtoto anayetarajiwa kuzaliwa” amesisitiza.

Aidha, Mhe. Telack amesisitiza umuhimu wa kuimarisha sekta ya kilimo kupitia mashamba darasa kuanzia ngazi ya kijiji hadi kata, ili kutoa elimu sahihi kwa wananchi juu ya uzalishaji wa mazao ya chakula na bustani ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Vilevile,amewahimiza Maafisa Elimu kuhakikisha shule zote zinatenga maeneo ya wanafunzi kujifunzia kazi za mikono ikiwemo kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo ya chakula ili watoto wapate chakula cha mchana na kujifunza kazi za mikono na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuandaa kizazi kinachowajibika na kinachothamini kilimo.
“Niwaombe sana kila mmoja kwenye nafasi yake asimamie vizuri ili tuweze kwenda sambamba. Kila mmoja akisimama vizuri tunaamini scorecard zetu zitakuwa kijani. Twende tukajenge lishe za wananchi wetu ili kupunguza sababu za wananchi kwenda hospitali mara kwa mara bila sababu za msingi,” ameeleza.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa Bi. Zuwena Omary amesisitiza uanzishwaji na ufuatiliaji wa mashamba darasa kuanzia ngazi za vijiji na kata ili kutoa fursa kwa wananchi kujifunza namna ya uzalishaji bora wa mazao ya chakula na bustani kwa tija ya kuongeza upatikanaji wa chakula na kuimarisha afya za wanajamii.

Afisa Lishe wa Mkoa Bi. Juliana Chikoti ameeleza kuwa kwa mwaka 2024/25 Mkoa umefanikiwa kutumia fedha kiasi cha shilingi milioni 311 kati ya milioni 376 zilizotengwa kwa ajiri ya kuratibu shughuki za huduma za lishe sawa na 86% na kubainisha changamoto kuu zinazokabili sekta hiyo ni pamoja na utoaji wa fedha za Lishe kwa wakati, ongezeko la watoto wanaozaliwa na uzito pungufu, upungufu wa unga wenye virutubisho, na idadi ndogo ya watoto wanaopata chakula shuleni.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa