Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, amefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali itakayopitiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 katika Wilaya ya Ruangwa, leo Aprili 4, 2025.
Miradi aliyotembelea ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Mwilali yenye urefu wa mita 650, mradi wa dampo salama uliyopo Kijiji cha Lipande, vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja katika Shule ya Msingi Dodoma, mradi wa maji katika Kijiji cha Mpara kata ya Likunja, ujenzi wa kituo cha polisi Nandagala, ujenzi wa kituo cha afya Namakuku, na ujenzi wa shule ya sekondari ya Namakuku.
Katika ukaguzi huo, Mhe. Telack ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa maagizo ya kukamilishwa kwa miradi ambayo bado haijafikia asilimia 100 ya utekelezaji.
Aidha, amesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unapaswa kuendana na thamani ya fedha na kuzingatia muda uliopangwa, hasa ikizingatiwa kuwa ni miradi inayotarajiwa kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru mnamo tarehe 28 Mei, 2025.
“Kasi ya ujenzi ni nzuri, lakini nataka kuona miradi yote imekamilika kwa viwango stahiki kabla ya ujio wa Mwenge,” amesema Mhe. Telack.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa imekuwa na faida kubwa kwa kuwa imesaidia kufuatilia kwa karibu maendeleo ya miradi ya wananchi, kutoa maelekezo ya kuboresha utekelezaji, na kuhakikisha kuwa miradi hiyo itakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, jambo ambalo litaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii na kukuza maendeleo ya Wilaya ya Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa