Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga, amewapongeza wajasiriamali wa Wilaya ya Ruangwa kwa kuwa na vifungashio bora vya bidhaa zao katika maonesho ya Nane Nane. Mhe. Ndemanga ameyasema hayo leo, tarehe 6 Agosti 2024, alipotembelea banda la Ruangwa kama mgeni rasmi wa maonesho ya Nanenane kanda ya kusini katika Viwanja vya Ngongo, Lindi.
Amewatia moyo wajasiriamali hao kwa ubunifu wao na kusema kwamba mara nyingi kumekuwa na mfanano wa vifungashio katika mabanda mbalimbali, lakini Ruangwa wamejipambanua kwa utofauti wao na kuwapa pongezi nyingi.
Aidha, Mhe. Ndemanga amewapongeza Mbwemkuru AMCOS kwa kazi nzuri ya kusimamia ushirika huo na kutoa wito kwa vyama vingine vya ushirika kujifunza kutoka kwao. Ametoa pongezi hizo baada ya kupokea maelezo na elimu ya ushirika kutoka kwa Katibu wa Mbwemkuru AMCOS, Ndugu Shabani Rutuba, aliyekuwa katika banda la Ruangwa akitoa elimu kuhusu ushirika, stakabadhi ya ghala, na mfumo wa masoko wa TMX.
Ndugu Rutuba ameeleza kuwa kwa msimu huu wamekusanya jumla ya kilo 1,947,524 za ufuta na kupata mapato ya Tsh 6,687,833,538, na hivyo kuwa AMCOS kinara katika makusanyo ya ufuta kwa Wilaya ya Ruangwa.
Ikumbukwe, maonesho ya Nane Nane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wajasiriamali kuonyesha ubunifu na ubora wa bidhaa zao. Ufanisi wa wajasiriamali wa Wilaya ya Ruangwa katika kubuni vifungashio bora ni mfano mzuri wa jinsi maonesho haya yanavyotoa fursa kwa washiriki kuboresha bidhaa zao na kuongeza ushindani katika soko. Mhe. Ndemanga amewahimiza wajasiriamali hao kuendelea kushiriki kikamilifu katika maonesho kama haya, ambayo yanaongeza uelewa na kujenga uwezo wa wajasiriamali kuboresha biashara zao na kuchangia maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya na nchi kwa ujumla.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa