Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ruangwa, Mwl. George Mbesigwe, amemkabidhi fomu ya uteuzi Mohamed Said Makota, mgombea wa nafasi ya Ubunge kupitia Chama cha MAKINI leo tarehe 23 Agosti 2025.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ruangwa iliyopo kwenye Jengo la Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, huku yakihudhuriwa na mashuhuda wachache wakiwemo wafuasi wa chama hicho.
Makota sasa anatakiwa kukamilisha taratibu za kisheria na kurejesha fomu hizo kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa uteuzi, hatua inayoongeza hamasa ya kisiasa jimboni humo.
Aidha, Mwl. Mbesigwe amewataka wagombea wote kuzingatia masharti na ratiba zilizotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), akisisitiza kuwa ofisi yake ipo wazi kwa kila mgombea bila upendeleo.
Kwa upande wake, Makota ameonesha furaha kwa kupata nafasi hiyo na amesisitiza dhamira yake ya kuwaletea wananchi wa Ruangwa maendeleo endapo atateuliwa na kuchaguliwa kuwa Mbunge.
Tukio hilo linaongeza msisimko wa kisiasa, huku wagombea kutoka vyama vingine vya siasa wakitarajiwa kuchukua na kurejesha fomu zao ndani ya muda uliopangwa na INEC.
Kwa mujibu wa ratiba ya kitaifa, zoezi la kuchukua na kurejesha fomu linaendelea hadi tarehe 27 Agosti katika majimbo yote nchini, kabla ya uteuzi rasmi na kuanza kwa kampeni.
Zoezi hili ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa