Mgogoro wa mirathi uliokuwa ukiikumba familia ya Abdallah Chitanda katika kijiji cha Nandagala “B,” Kata ya Nandagala, wilayani Ruangwa, umesuluhishwa kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, leo Februari 27, 2025, katika viwanja vya stendi ya Nandagala.
Mgogoro huo ulihusu mgawanyo wa mashamba ya marehemu, ambapo ndugu sita wa familia hiyo walishindwa kufuata utaratibu wa kisheria, hali iliyopelekea mdogo wao wa mwisho kukosa mirathi kabisa, huku kaka yao mkubwa akijitwalia karibu nusu ya eneo lote na kujimilikisha mwenyewe, Kupitia msaada wa kisheria uliotolewa leo pande zote zimekubaliana kutekeleza mgawanyo wa mali kwa mujibu wa sheria, hatua iliyorejesha amani ndani ya familia.
Aidha, Mmoja wa wanafamilia Bi. Fatuma Abdallah, amepongeza juhudi za Serikali kupitia kampeni ya Mama Samia kwa kuwawezesha kupata haki zao bila gharama za kisheria.
“Msaada huu umeokoa familia yetu na kuzuia uhasama uliokuwa ukianza kujengeka kutokana na mgogoro wa mirathi”. Amesema Bi. Fatuma
Naye, Mratibu wa kampeni hiyo Wilaya ya Ruangwa Ndugu. Antony Elias amesema msaada wa kisheria unaendelea kutolewa kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali, ikiwemo mirathi, ardhi, ndoa, na masuala mengine ya kisheria, huku elimu ikitolewa kwa kila mwananchi, lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata haki kwa mujibu wa sheria na kuimarisha mshikamano katika jamii.
Hata hivyo, Wananchi wa Nandagala wamehimizwa kutumia fursa hiyo ya msaada wa kisheria ili kuepusha migogoro na kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kampeni ya Mama Samia Legal Aid inaendelea kutekelezwa wilayani Ruangwa, ikiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kisheria na huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi, ili kuimarisha utawala wa sheria na kupunguza migogoro katika jamii.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa