Mwalimu Uzima Justine ameshauri serikali za vijiji kubuni vyanzo vya mapato ya kijiji ili viweze kuwasaidia katika kuanzisha na kuendeleza miradi katika maeneo yao.
Alisema "kuwa na vyanzo vya mapato vya kijiji kutasaidia kuchochea maendeleo zaidi katika vijiji vyao kwasababu kutakuwa na miradi wanayotekeleza wenyewe kwa fedha za ndani".
Ameyasema hayo leo 17/06/2022 wakati wa mafunzo ya utawala bora yanayoratibiwa na Jukwaa la Elimu ya Uraia Tanzania (CETA) yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya mjini Ruangwa.
Alisema "kupitia vyanzo hivyo vya mapato, watakusanya mapato ya kijiji ambayo wanapaswa kuyatumia vizuri kwa kufuata sheria".
"Hizo si fedha za matumizi yenu binafsi bali ni fedha kwa ajili ya maendeleo ya kijiji, msije kuwa mnagawana posho tu, wananchi wanatakiwa kujua kinachokusanywa na kinavyotumika"
Pia aliwataka kuwa na sheria ndogo na kuzizingatia sheria hizo kwani zitawaongoza katika kutenda haki kwa wananchi wao.
Naye mshiriki kutoka Namkatila ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Bi. Mwanahamisi Soko aliushukuru uongozi wa Jukwaa la Elimu ya Uraia Tanzania (CETA) kwa kuwapatia mafunzo hayo na kuwaomba washiriki wengine kupeleka mrejesho kwa wajumbe wengine wa serikali za kijiji ambao hawajapata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo.
Alisema Bi. Mwanahamisi, "mafunzo tuliyoyapata ni urithi mkubwa kwani yatadumu kwasababu si kitu cha kuisha na pia tutatumia elimu hii katika utendaji ili vijiji viwe bora zaidi".
Pia Bi Mwanahamisi alisema suala la uongozi huwa si la milele, uongozi unabadilika badilika hivyo aliuomba uongozi wa CETA kutoishia kipindi hiki kwamba wawe wanatoa mafunzo kila uongozi unapobadilika ili vijiji vyote vizidi kuwa bora.
Mafunzo haya yanaratibiwa na Jukwaa la Elimu ya Uraia Tanzania (CETA) yanayohusisha wenyeviti wa vijiji, Watendji wa Vijiji na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Vijiji na yamelenga kuwafikia viongozi wa serikali za vijiji 90 katika Wilaya ya Ruangwa.
Mpaka sasa washiriki 445 wamepatiwa mafunzo na vijiji 67 vimeshiriki kwa ukamilifu mafunzo hayo.
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa