Mameneja na wahasibu 130 wa RUNALI kutoka Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale wamehitimu mafunzo ya PAVU yaliyolenga kuongeza ujuzi katika usimamizi na uadilifu wa fedha za vyama vya ushirika (Amcos).
Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia Oktoba 10 hadi 24, 2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, yalihusisha washiriki 130 wakiwemo wanaume 127 na wanawake 3. Lengo lake kuu lilikuwa kuwajengea uwezo wa kitaaluma wahasibu na mameneja ili kuimarisha uwazi, uadilifu na utunzaji sahihi wa kumbukumbu za kifedha katika Amcos.
Aidha, viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mh. Hassan Ngoma, pamoja na Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika cha Moshi (MoCU) na viongozi wa RUNALI, wamesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo katika kuboresha usimamizi wa vyama hivyo.
Vilevile, viongozi hao wamepongeza hatua ya kutoa mafunzo hayo wakieleza kuwa yatasaidia kuzuia hati chafu, kuongeza ufanisi wa kifedha na kuimarisha maendeleo ya wakulima kupitia Amcos.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Hassan Ngoma, amewataka wahasibu na mameneja kutumia maarifa waliyopata kuboresha ufanisi katika vyama vyao vya ushirika.
“Elimu hii mliyoipata isiishie kwenye vyeti pekee, bali iwe chachu ya mabadiliko kwenye usimamizi wa fedha na kumbukumbu za Amcos. Tunataka kuona vyama vyenu vikisimamia kwa uwazi, uadilifu na kwa manufaa ya wakulima,” amesema Mh. Ngoma.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kama RUNALI na MoCU katika kuhakikisha elimu ya fedha na usimamizi bora inawafikia viongozi wote wa vyama vya ushirika nchini.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yamechukuliwa kuwa hatua muhimu ya kuleta mageuzi chanya katika sekta ya ushirika, hasa katika kuhakikisha matumizi sahihi na yenye tija ya fedha za wakulima.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa