Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema wakazi wa Wilaya ya Ruangwa hawana deni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na kazi kubwa aliyoifanya wilayani humo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara leo 15 Machi 2025 katika Kijiji cha Narungombe, Wilaya ya Ruangwa, Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia amewezesha upatikanaji wa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta za kilimo, afya, elimu, miundombinu na nyanja nyingine muhimu.
Aidha, amesema Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji wa shilingi bilioni 119 kutoka Mto Nyangao, ambao utahudumia vijiji 34 vya Ruangwa na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa uhakika. Amesisitiza kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa kutatua changamoto ya maji inayosababishwa na chumvi nyingi ardhini kutokana na sababu za kijiografia.
“Nitaendelea kufanya kazi na nyinyi usiku na mchana, jua na mvua, hadi kuhakikisha Ruangwa inafanikiwa zaidi,” ameahidi Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameshuhudia wanachama 24 wa ACT-Wazalendo wakihama na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwemo aliyekuwa Katibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo Wilaya ya Ruangwa, Hammis Selemani Chikanga, Diwani wa Kata ya Mbwemkuru, Ismail Ali Mbwerei, na Katibu wa Vijana, Omary Kitunguu.
Kwa niaba ya wenzake, Hammis Chikanga amesema wameamua kujiunga na CCM ili kuunga mkono jitihada na kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa