Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Mhe. Kassim Majaliwa, amewataka wananchi wa Ruangwa kuendelea kuwa na matumaini, huku wakijivunia maendeleo makubwa yanayoendelea katika Wilaya yao, akizungumza leo tarehe 13 Septemba katika Tamasha la Hamasa Day Ruangwa 2024, lililofanyika katika Viwanja vya Madini, Kilimahewa, Majaliwa ameweka wazi mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu na miundombinu.
Amesema kuwa, licha ya Ruangwa kuwa Wilaya changa, Serikali imeweka kipaumbele kwenye elimu kwa kuhakikisha kila kata ina shule za sekondari. "Kata zote za Ruangwa zina shule za sekondari, na hivi karibuni tumepokea shilingi milioni 900 kutoka kwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari Namichiga na Namakuku," amesema Majaliwa. Ameongeza kuwa juhudi hizi zinaonesha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha kizazi kijacho kinapata elimu bora na mazingira mazuri ya kujifunza.
Mhe. Majaliwa pia amesisitiza kuwa maendeleo ya Ruangwa si ya watu wachache bali ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali na wananchi, amesema kuwa, kama mwakilishi wa wananchi, anahakikisha kuwa mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
“Maendeleo tunayoyaona Ruangwa ni ushahidi wa ushirikiano wetu, ni jukumu letu sote kuendelea kuunga mkono juhudi hizi kwa vitendo,” amesisitiza.
Kwa kuunga mkono juhudi za kukuza afya, Mhe. Majaliwa amewaalika wananchi kushiriki katika Ruangwa Marathon, itakayofanyika kesho, Septemba 14, ameeleza kuwa mbio hizo ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Samia katika kuhamasisha afya bora kupitia mazoezi, Mazoezi ni sehemu muhimu ya maisha yetu na Ruangwa Marathon ni fursa kwa sisi sote kushiriki.
Katika hatua nyingine, Majaliwa ametangaza kuwa Wasafi Festival 2024 itazinduliwa rasmi Ruangwa tarehe 14 Septemba, kabla ya kuendelea katika Mikoa mingine nchini. Uzinduzi huo unaleta fursa za kiuchumi na burudani, na kuongeza sifa za Ruangwa kama kitovu kipya cha matukio makubwa ya kijamii.
Ikumbukwe, Kwa miaka mingi, Ruangwa imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kimaendeleo, hasa katika sekta za elimu na miundombinu, hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, Wilaya imepata mafanikio makubwa, kupitia uwekezaji katika elimu na miundombinu, Serikali imepiga hatua za kuimarisha ustawi wa wananchi. Ikiwa juhudi hizi zitaendelea, Ruangwa inaelekea kuwa miongoni mwa Wilaya zenye maendeleo makubwa nchini.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa