Msimamizi wa Uchaguzi Mkuu Jimbo la Ruangwa, Mwl. George Mbesigwe, amefungua rasmi mafunzo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata kwa kata zote 22 za Jimbo hilo mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Shule ya Wasichana Ruangwa leo tarehe 04 Agosti 2025.
Mafunzo hayo yamepangwa kufanyika kwa muda wa siku tatu, yakilenga kuwaandaa wasimamizi hao kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria na taratibu. Sambamba na mafunzo hayo, wasimamizi wote wamekula viapo viwili muhimu, kiapo cha kujitoa uanachama au kutokuwa mwanachama wa chama cha siasa na kiapo cha kutunza siri.
Aidha, akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Mwl. Mbesigwe amesisitiza kuwa ufanisi wa uchaguzi unategemea kwa kiasi kikubwa uelewa wa kina wa sheria, kanuni, miongozo na taratibu zinazotawala mchakato wa uchaguzi. Ameeleza kuwa kila msimamizi ana wajibu wa kuhakikisha mchakato unakwenda kwa haki na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Mwl. Mbesigwe, ni wajibu wa kila msimamizi kuhakikisha kuwa kila hatua ya uchaguzi inazingatia misingi ya uwazi, usawa na uaminifu.
“Wasimamizi wa uchaguzi ni nguzo muhimu katika kulinda amani, demokrasia na haki ya kila Mtanzania kupiga kura, lazima mfanye kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo,” amesema Mwl. Mbesigwe.
Vilevile, amewataka wasimamizi hao kuzingatia kwa makini mafunzo wanayopewa, huku akisisitiza kuwa uelewa mdogo wa taratibu unaweza kuathiri mwenendo mzima wa uchaguzi. Ameongeza kuwa hatua yoyote ya uzembe au ukiukwaji wa taratibu inaweza kusababisha athari kubwa kwa jamii.
Hali kadhalika, Mwl. Mbesigwe amesisitiza kuwa viapo walivyokula si vya kawaida, bali ni ahadi ya kisheria inayowalazimu kuwa waaminifu, kutunza siri na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa. Amewataka kila mmoja kutumia muda wa mafunzo kujifunza, kuuliza na kujadiliana ili kufanikisha uchaguzi wa haki.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea uwezo wasimamizi wa uchaguzi kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wao, mazingira ya kazi, na namna ya kushughulikia changamoto mbalimbali wakati wa mchakato wa uchaguzi, huku dhamira kuu ikiwa ni kuhakikisha uchaguzi huru, haki na wa kuaminika.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa