Mafunzo maalum ya tathmini na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo yamefanyika leo, Septemba 17, 2024, katika Shule ya Sekondari Ruangwa yakihusisha Watendaji wa Kata zote 22 za Wilaya ya Ruangwa, mafunzo hayo yameandaliwa na Idara ya Mipango na Ufuatiliaji, yakilenga kuboresha ufanisi na uwajibikaji katika usimamizi wa miradi, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo Wilayani humo.
Katika mafunzo hayo, watendaji wa kata wamepatiwa mikataba inayowapa mamlaka ya kusimamia moja kwa moja miradi ya maendeleo ndani ya kata zao. Hatua hii imelenga kuhakikisha kuwa watendaji wanasimamia kwa ufanisi miradi yote inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ndugu Frank Chonya amehitimisha mafunzo hayo kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya watendaji, akieleza kuwa mafunzo hayo yatakuwa msingi wa maendeleo endelevu, amehimiza watendaji kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi na uwajibikaji ili miradi yote itekelezwe vizuri kwa manufaa ya wananchi.
Sambamba na hayo, Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali wametoa nasaha zao, wakiwapongeza watendaji kwa kujituma na kushirikiana. Wamesisitiza kuwa mafunzo kama hayo ni muhimu katika kuwaongezea ujuzi na maarifa ya kusimamia miradi kwa viwango vya hali ya juu.
Kwa upande wao , Watendaji wa Kata, wameonesha kuridhika na mafunzo hayo, wakieleza kuwa yamewapa ujuzi muhimu wa kusimamia miradi ya maendeleo. Wamesema, "Mafunzo haya yametupa uwezo wa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati, na tupo tayari kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ili kuleta maendeleo katika kata zetu." Amesema Mtendaji wa Kata ya Mbwemkuru
Katika hali ya sasa, semina kama hizi zimeimarisha uwezo wa watendaji wa kata katika kusimamia miradi ya maendeleo, tofauti na miaka ya nyuma ambapo ukosefu wa mafunzo kama haya ulisababisha changamoto nyingi. Ili kuona mafanikio endelevu, ni muhimu mafunzo ya mara kwa mara yaendelee kutolewa, huku ushirikiano kati ya watendaji na viongozi wa Halmashauri ukiimarishwa kwa ajili ya maendeleo ya baadaye ya Wilaya ya Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa