Ujio wa Madaktari bingwa wa Mama Samia kwa awamu ya pili ya huduma zao umekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Ruangwa, huku tukio la kuokoa maisha ya mama mjamzito likitoa picha kamili ya umuhimu wa huduma hizo za kibingwa.
Jumanne, Septemba 17, 2024, madaktari hao wamefanikiwa kufanya upasuaji wa dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa kwa mama aliyekuwa na mimba iliyotunga nje ya mji wa mimba. Hali hiyo ilimsababisha kutokwa na damu ndani kwa ndani, hali iliyohatarisha maisha yake, licha ya hali yake kuwa mbaya, upasuaji huo umefanywa kwa mafanikio makubwa, na hadi sasa mgonjwa huyo anaendelea vizuri.
Kwa upande wake, Mdogo wa mgonjwa huyo, Bi Maua Ally, ametoa shukrani zake kwa madaktari hao, akisema kwamba hali ya dada yake ilikuwa mbaya sana, lakini jitihada za haraka za madaktari zimeokoa maisha yake. "Tulikuwa tumeingiwa na hofu kubwa, lakini sasa tunashukuru, hali ya dada yangu inatia matumaini na tunawaombea madaktari kila la kheri," amesema Bi Maua kwa hisia.
Madaktari hao wa Mama Samia wapo katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa kwa muda wa siku sita, kuanzia Septemba 16 hadi Septemba 21, 2024. Lengo kuu la ujio wao ni kusogeza huduma za kibingwa na bobezi karibu na wananchi wa Ruangwa na maeneo jirani, huduma ambazo zimekuwa ngumu kupatikana kwa urahisi kwa jamii ya vijijini.
Kwa miaka mingi, wananchi wa Ruangwa walikumbana na changamoto za upatikanaji wa huduma za kibingwa, jambo ambalo liliwalazimu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo. Hata hivyo, ujio wa madaktari hawa bingwa wa Mama Samia ni faraja na ni dalili njema kwa mustakabali wa afya za wananchi wa Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa