Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa wamepewa mafunzo ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mafunzo hayo yamefanyika leo, Mei 14, 2025, katika bwalo la Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruangwa, yakihusisha pia wakufunzi kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Maafisa TEHAMA, Maafisa Ugavi pamoja na Maafisa Waandikishaji wa ngazi ya Jimbo.
Aidha, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha maafisa husika kupata uelewa wa kina kuhusu taratibu sahihi za uandikishaji wapiga kura, sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa inayotumika katika usajili huo. Washiriki wameelekezwa namna ya kutumia Mfumo wa Usajili wa Wapiga Kura (VRS), ambao umeboreshwa ili kuongeza usahihi wa taarifa na kupunguza changamoto za kiufundi wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Vilevile, mada mbalimbali zimewasilishwa kwa lengo la kuwajengea ujuzi wa vitendo washiriki hao, ikiwa ni pamoja na ujazaji wa fomu za usajili kwa usahihi, utunzaji wa vifaa vya kazi, na mbinu za kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza kwenye vituo vya uandikishaji. Washiriki pia wamekumbushwa umuhimu wa kushirikiana kwa karibu na viongozi wa maeneo yao ili kuongeza mwitikio wa wananchi kushiriki zoezi hilo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili kwa Wilaya ya Ruangwa unatarajiwa kuanza rasmi Mei 16 na kukamilika Mei 22, 2025. Katika kipindi hicho, wananchi wenye sifa ya kupiga kura wanahimizwa kujitokeza katika vituo vilivyopangwa ili kujiandikisha, kurekebisha taarifa zao au kuhakiki taarifa zilizopo.
Hata hivyo, Tume imeeleza kuwa dhamira yake ni kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura anapata fursa ya kuwa katika daftari hilo.
Kwa upande mwingine, Maafisa Waandikishaji walioshiriki mafunzo hayo wametakiwa kuzingatia maadili, weledi na uaminifu katika kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa mustakabali wa taifa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa