Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kupitia Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeendesha mafunzo kwa Maafisa Ugani Mifugo 19 watakaoshiriki katika zoezi la kitaifa la utambuzi na uchanjaji wa mifugo. Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 11 Julai 2025 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo watendaji hao katika matumizi ya mfumo wa kisasa wa uchanjaji na utambuzi wa mifugo.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Chonya, amewataka Maafisa Ugani kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kushirikiana kwa karibu na wafugaji. Amesisitiza kuwa kampeni hiyo ya kitaifa, inayotolewa kwa ruzuku na Serikali ya awamu ya Sita, inalenga kuhakikisha wafugaji wanapata huduma bora ili kuboresha afya ya mifugo na kuinua kipato cha kaya za wafugaji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kampeni ya chanjo kitaifa imezinduliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Simiyu, ikiwa ni hatua muhimu ya kitaifa kulinda afya ya mifugo.
Aidha, ng’ombe wanatarajiwa kuchanjwa dhidi ya homa ya mapafu kwa bei ya ruzuku ya shilingi 500 kwa mnyama; mbuzi na kondoo watachanjwa dhidi ya Sotoka kwa shilingi 300 kwa mnyama; huku kuku wakichanjwa dhidi ya kideri, ndui na mafua makali kwa gharama zote kufidiwa na Serikali.
Vilevile, Serikali imetangaza kutoa vitendea kazi kwa wataalamu wa mifugo, vikiwemo vishikwambi na usafiri wa pikipiki, ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa zoezi la uchanjaji na huduma kwa wafugaji.
Mpaka sasa, Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imepokea dozi 110,000 za chanjo ya kuku aina ya Tatu Moja, dozi 3,000 za homa ya mapafu (CBPP) kwa ng’ombe, na dozi 9,500 za Sotoka kwa mbuzi na kondoo. Tayari zoezi la chanjo ya kuku limeanza kutolewa, ambapo hadi sasa wafugaji 2,036 wamefikiwa na jumla ya kuku 35,773 wamechanjwa.
Kwa sasa, maandalizi ya mwisho yanaendelea, yakiwemo ukamilishaji wa mfumo wa utambuzi wa mifugo na usambazaji wa vifaa vya uchanjaji, ili chanjo za homa ya mapafu na Sotoka ziweze kuanza kutolewa mwezi huu wa saba.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa