"Tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kuwaongoza na kuwasimamia watoa huduma ya upasuaji katika kituo chetu hiki na mpaka kufikia leo hii wagonjwa zaidi ya 70 wamepatiwa huduma hiyo na kutoka wakiwa salama salmini, lakini pia pongezi kubwa kwa yule mteja wetu wa kwanza kabisa ambaye alikuwa na imani kubwa na watoa huduma wa kituo chetu cha Afya na kuwa balozi mzuri kwa wananchi wengine kuwaaminisha ya kwamba Wataalamu wetu wa Afya katika kituo hiki wanatoa huduma ya upasuaji kwa weredi mkubwa"
Hayo yamebainishwa leo Juni 17, 2024 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mhe. Andrew Chikongwe ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika Kikao cha maadhimisho ya kutimiza mwaka mmoja tangu kuanza kutolewa huduma ya upasuaji katika Kituo cha Afya Nandagala, kilichofanyika katika kituo hicho.
Kituo hicho kimefunguliwa December 27, 2016 na kuanza kutoa huduma kama Zahanati na ilipofika mwaka 2022, kikaboreshwa zaidi na kuanza kutoa huduma kwa jamii kama Kituo cha Afya.
Mpaka sasa Kituo kina jumla ya Watumishi 14 na zaidi ya wananchi 20,000 wanapata huduma kupitia Kituo hicho, huduma zinazotolewa ni pamoja na huduma ya
kujifungua (kwa njia ya kawaida na upasuaji) ambapo zaidi ya wakinamama 700 wamejifungulia katika kituo hicho, huduma ya kuona wagonjwa wa nje(OPD), huduma ya nasaha na upimaji wa VVU, huduma ya IPD(Wodi ya wakibaba, wakimama na watoto) na huduma nyingine nyingi.
Huduma ya upasuaji kwa mara ya kwanza ilifanywa na Dkt. Paul Christian Mbinga akishirikiana na Wataalam wengine kwa Bi Fikiri Bakari mkazi wa kijiji cha Ng'au mnamo Juni 12, 2023.
Aidha, Mhe. Chikongwe amemuomba Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Feisal Said kuhakikisha Kituo cha Afya Nandagala kinakuwa na daktari bingwa wa kinywa na meno na hii ni kufuatia hatua ya kituo hicho kupokea kiti maalum kwa ajili ya huduma hiyo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Feisal Said ametoa wito kwa Watumishi wa Kituo cha Afya Nandagala kufanya kazi kwa bidii, kupambana na kushirikiana vyema na Wataalam kutoka ngazi ya Wilaya ili kuleta mafanikio makubwa.
"Mkitaka mfanikiwe fanyeni makubwa kazini na siri ya kufanikiwa ni kupambana tu" amesema Dkt. Feisal.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa