Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imefanya kongamano maalum la ukusanyaji wa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050. Kongamano hilo, limewakutanisha watu kutoka makundi mbalimbali katika jamii na limefanyika leo, Julai 29, 2024, katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inalenga kuendeleza mafanikio ya Dira ya 2025 na kuleta maendeleo endelevu kwa muda mrefu. Malengo ya Dira ya 2050 ni pamoja na kukuza uchumi wenye ushindani kimataifa, kuongeza ustawi wa jamii, kuimarisha miundombinu, huduma za kijamii, na kulinda mazingira. Serikali inashirikisha wadau mbalimbali katika mchakato wa kuandaa mpango huo ili kuhakikisha kuwa unakidhi mahitaji na matarajio ya Watanzania.
Aidha, Wadau wa maendeleo na makundi mbalimbali ya wananchi wa Wilaya ya Ruangwa wamejitokeza na kutoa maoni na matamanio yao kuhusu namna wanavyotamani kuiona Tanzania ifikapo mwaka 2050. Baadhi ya maoni hayo ni pamoja na; kuwekeza katika Teknolojia kuanzia shule za msingi hususani katika matumizi ya tehama, kutoa huduma za afya bure kwa wajawazito ifikapo 2050, kuongeza wataalamu katika sekta ya kilimo kuanzia ngazi ya kijiji, kudumisha zaidi amani na usalama wa Taifa ili nchi izidi kuwa salama, kupunguza bei ya gesi na umeme ili Watanzania wote watumie nishati safi ifikapo 2050, Kuwe na gredi ya Taifa ya maji kama ulivyo umeme, kuongeza ajira kwa vijana ili kuwaokoa na janga la madawa ya kulevya, na Taifa lijikite kwenye uwekezaji wa viwanda ili kuongeza soko la ajira.
Ikumbukwe, Kongamano hilo limeonyesha jinsi ambavyo Serikali inathamini maoni ya wananchi katika mipango ya maendeleo ya Taifa. Ushirikishwaji huo ni muhimu kwa kuhakikisha kwamba mipango inayowekwa inakidhi mahitaji halisi ya jamii na kuchangia katika kujenga Tanzania yenye ustawi na maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2050.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa