Timu ya Kiwengwa FC kutoka Soko Kuu Ruangwa imetwaa ubingwa wa mashindano ya Jimbo Cup 2024 baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Stand United kutoka Stendi Kuu ya Mabasi, mchezo huo, umeochezwa leo Novemba 25, 2024, katika Uwanja wa Majaliwa Stadium majira ya saa 10 jioni, umemalizika kwa sare ya goli 1-1 kabla ya kuamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati, ambapo Kiwengwa FC wamefunga penati 3 dhidi ya 1 ya Stand United.
Mgeni rasmi wa fainali hiyo, Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ametoa zawadi ya shilingi milioni 5 kwa Kiwengwa FC kama mshindi wa kwanza wa mashindano hayo, Stand United, walioshika nafasi ya pili, wamepewa shilingi milioni 4 kama zawadi ya kushiriki mashindano hayo kwa mafanikio.
Aidha, timu ya Red Star kutoka kijiji cha Chikundi Kata ya Mandawa imepewa shilingi milioni 3 baada ya kushika nafasi ya tatu, huku Napoli FC kutoka kijiji cha Mbekenyera wakikabidhiwa shilingi milioni 1.5 kwa kushika nafasi ya nne.
Katika hotuba yake, Mhe. Majaliwa amesisitiza kuwa mashindano haya ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mshikamano wa kijamii, kuibua vipaji vya michezo, na kuhamasisha maendeleo ya vijana wilayani Ruangwa. Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya michezo ili kutoa fursa kwa vijana zaidi kuonyesha vipaji vyao.
Mashindano ya Jimbo Cup 2024, ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka, yameleta hamasa kubwa kwa wananchi wa Ruangwa, huku yakichangia maendeleo ya sekta ya michezo na kujenga mshikamano miongoni mwa jamii za maeneo mbalimbali ya wilaya. Mwaka huu, mashindano hayo yalivutia timu kutoka kata na vijiji mbalimbali, jambo linalodhihirisha ukuaji wa michezo katika ngazi ya wilaya.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa