Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Komredi Mohammed Kawaida, ametoa wito kwa vyama vingine kuiga mfano wa vijana wa CCM kutokana na uadilifu, nidhamu, uchapa kazi, utii na uzalendo wanaoonesha, ameyasema hayo leo Septemba 13, 2024, wakati wa Tamasha la Vijana lijulikanalo kama "Hamasa Day," lililofanyika katika uwanja wa Maonesho ya Madini, Wilaya Ruangwa.
Katika hotuba yake, Komredi Kawaida amewapongeza wana Ruangwa kwa hamasa kubwa waliyoonesha katika tamasha hilo, akisema kuwa wananchi wa Ruangwa wamependezesha hafla hiyo kwa namna isiyokuwa ya kawaida. "Hakika Ruangwa mmetisha sana, hamasa yenu ni ya kipekee, ni jambo zuri mnapaswa kuigwa na maeneo mengine," amesema Kawaida.
Aidha, tamasha hilo limeambatana na ufunguzi wa matawi mawili ya vijana wa CCM katika maeneo ya Alaala na kwa Mtota, Wilaya ya Ruangwa,komredi Kawaida amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuendelea kushikamana kwa nguvu ili kuleta maendeleo endelevu na kufanikisha malengo ya Chama Cha Mapinduzi, akiongeza kuwa vijana ni nguvu ya taifa.
Kwa kutazama historia ya Umoja wa Vijana wa CCM, ambao ulianzishwa mnamo mwaka 1978 baada ya kuunganishwa kwa vyama vya vijana wa TANU na ASP, umoja huo umeendelea kuwa nguzo muhimu kwa maendeleo ya vijana nchini. Kwa sasa, UVCCM inabaki kuwa chombo cha kuimarisha uzalendo na uongozi miongoni mwa vijana, huku ikitarajiwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa taifa kwa miaka ijayo. Suluhisho likiwa ni vijana kuendelea kupewa fursa zaidi na kuendelezwa ili wawe viongozi bora wa kesho.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa