Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kiwilaya kimefanyika Machi 6, 2024 katika viwanja vya shule ya msingi Likunja Kata ya Likunja wilayani Ruangwa ikiwa na kauli mbiu "Wekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo ya Taifa na Ustawi wa jamii" ambapo Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Katibu Tawala Wilaya Mhandisi Zuhura Rashidi kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa Mheshimiwa Zuwena Omari
Katibu Tawala Wilaya amepata nafasi ya kukutana na wajasiriamali pamoja na wataalamu wa idara ya Afya kitengo cha Ukimwi na Saratani ya Shingo ya kizazi na ameshiriki katika upimaji wa afya yake.
Katika hatua nyingine maadhimisho hayo yamehusisha harambee fupi kwa mwanafunzi mlemavu wa shule ya msingi Likunja Aisha Hassan Swalehe (16) anayesoma darasa la 7 na harambee hiyo imeongozwa na Katibu Tawala Wilaya na kwa upendo na huruma ya Wanawake hao wamemchangia mwanafunzi huyo kiasi cha fedha zaidi shilingi milioni moja.
Lakini pia Maadhimisho hayo yameudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wawakilishi kutoka NMB na CRDB, Viongozi wa dini mbalimbali, washiriki kutoka mashirika yasiyo ya serikali pamoja na vyombo vya usalama katika kuimarisha ulinzi na usalama katika sherehe hiyo.
Aidha, katika maadhimisho haya yameambatana na mada tofauti tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo "umuhimu wa wosia kwa wanawake" imetolewa na Shirika la msaada wa kisheria, "Wekeza kwa Mwanamke" mada hii imetolewa na CRDB, "Teleza kidigitali" mada hii imetolewa na NMB pamoja na " Wanawake kujali Afya zao kwani Afya ni mtaji" mada hii imetolewa na wataalamu kutoka idara ya Afya.
Katika hatua nyingine Diwani wa Kata ya Likunja Mhe. Issa Mussa Ngongonda ametoa shukrani kwa Kamati ya maandalizi ya sherehe ya Wanawake kwa mpangilio mzuri wa sherehe hizo kwani zimefana kweli kweli na kutoa rai kwa Wanawake kujiweka karibu na taasisi za kifedha ili kupata mikopo ambayo itasaidia kuendesha maisha yao na kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa kwa wakati sahihi ili kujikwamua katika dimbwi la umaskini.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa