Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omari ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kupata hati safi miaka mitano mfululizo kutoka mwaka wa fedha 2018/2019 hadi 2022/2023.
Pongezi hizo zimetolewa leo Juni 26, 2024 katika Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la kupitia na kujadili hoja za Mkaguzi wa hesabu za mwisho za mwaka wa fedha 2022/2023.
Aidha. Bi Zuwena amewasisitiza Viongozi na Watendaji wa Halmashauri kuilinda hati safi hiyo ili isije kuwa hati yenye mashaka au hati mbaya kwa mwaka wa 2023/2024.
Awali akiwasilisha taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa zinazoishia tarehe Juni 30, 2022/2023 Ndugu Donald Malick kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali Mkoa wa Lindi, amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ilikuwa na hoja za ukaguzi 25 kati ya hizo 13 zimeshatekelezwa na kufungwa, hoja 10 zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na hoja 2 hazijatekelezwa.
Kwa Upande wa Mfuko wa pamoja wa Afya (Basket Fund) kulikuwa na hoja 3 kati ya hizo 2 zimefungwa na hoja 1 ipo katika hatua ya utekelezaji, halikadhalika Mfuko wa Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu kulikuwa na hoja 3 ambapo 1 imetekelezwa na 2 zipo katika hatua za utekekezaji.
Kutokana na hali hiyo Bi. Zuwena amewataka Madiwani na Watendaji wa Halmashauri kuharakisha kutafuta vielelezo vya hoja zilizobakia na kuziwasilisha ofisi ya Mkaguzi ili hoja hizo zifungwe.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Hassan Ngoma ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha mwaka ujao wa fedha Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa isiwe na hoja za ukaguzi.
Nae, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mhe. Andrew Chikongwe ametoa pongezi kwa Madiwani kwa kusimamia fedha za Halmashauri hasa upande wa miradi ya maendeleo na kutoa wito kuendelea kushirikiana ili kuendelea kufanya mambo mazuri na ya kuleta maendeleo katika Kata na Halmashauri kwa ujumla.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa