Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Eng. Mwajuma Waziri, ametembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima vitano vya maji safi na salama unaotekelezwa Wilayani Ruangwa, lengo likiwa ni kuboresha huduma za maji kwa wananchi, mradi huo, unaogharimu Shilingi milioni 325, umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo kila Mbunge amepewa visima 5 jimboni kwake lengo likiwa ni kufikisha huduma ya maji katika maeneo ambayo hayakuwa na huduma hiyo kabisa.
Ziara hiyo ya kikazi imefanyika leo, Desemba 13, 2024, ikihusisha wakuu wa Idara, wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, na viongozi mbalimbali wa Wilaya. Katika Wilaya ya Ruangwa, vijiji vitano vinavyonufaika na mradi huo ni Mmawa, Namkatila, Mtawilile, Njawale, na Mpara, ambapo jumla ya wakazi 4,195 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Waziri ameeleza kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama vijijini unafika kila kona ya Tanzania.
“Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kumaliza changamoto ya maji katika vijiji vingi vya Wilaya ya Ruangwa na hata Wilaya za jirani,” amesema Eng. Waziri.
Aidha, Eng. Waziri ametoa ahadi kwa wananchi wa Kijiji cha Mmawa, kilichopo Kata ya Nandagala, kuwa mradi huo utaanza kutoa huduma rasmi kabla ya Sikukuu ya Krismasi, Desemba 25, 2024.
Hata hivyo, Mradi huo wa kimkakati ni miongoni mwa hatua za Serikali za kuwasaidia Wabunge kutekeleza miradi ya maendeleo katika majimbo yao, kwa manufaa ya wananchi waliowachagua. Eng. Waziri amewasihi wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha miradi kama hiyo inahifadhiwa na kutumika kwa ufanisi.
Nao, Wakazi wa vijiji vilivyonufaika wameshukuru kwa hatua hiyo na kueleza kuwa itabadilisha maisha yao kwa kuwaondolea changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Bwana Rashidi Juma amesema, “tunaishukru sana Serikali yetu inayoongozwa na mama Samia lakini pia Mbunge wetu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, hakika tunajivunia sana mradi huu, ukianza kutumika watu wote tutakuwa na amani maana shida ya maji itakuwa imeondoka kwenye vijiji vyetu”. amesema Juma
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa