Kambi maalum kwa ajili ya matibabu ya macho imefanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa kuanzia tarehe 8 Julai 2024 hadi leo Julai 19, 2024, Kambi hiyo yenye lengo la kusogeza huduma ya upasuaji wa macho kwa wananchi, imeandaliwa na Serikali ya Tanzania ikishirikiana na shirika la Eye Corps, lenye makao yake makuu nchini Marekani.
Katika kambi hiyo, wagonjwa 728 wamepata huduma za uchunguzi wa macho, kati yao wagonjwa 272 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho. Upasuaji huo umefanywa na Madaktari bingwa kutoka Tanzania, India, na Marekani. Huduma hii imetolewa bila malipo yoyote kwa wagonjwa, hatua ambayo imepokelewa kwa shukrani kubwa na jamii, ikumbukwe shirika la Eye Corps limeingia ubia na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa huduma za matibabu ya macho katika Mikoa ya Lindi, Ruvuma (Songea), na Kilimanjaro.
Aidha, Dkt. Mwita Machage, ambaye ni Mratibu wa Huduma za Macho Mkoa wa Lindi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Sokoine, ameeleza jinsi huduma hiyo ilivyofanikiwa kuwafikia watu wengi, lakini pia amehimiza watu kujenga tabia ya kupima macho mara kwa mara, ili kufahamu afya ya macho yao. Pia, ametoa shukrani kwa wananchi wa Ruangwa kwa kujitokeza kwa wingi kupima macho na kupata matibabu.
Sambamba na hayo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Feisal Said, ameishukuru Serikali kwa kuwezesha huduma hiyo iliyodumu kwa siku 11 na kufanikisha kurudisha furaha kwa wakazi wengi wa Ruangwa.
"Kambi hii imesaidia sana maana wagonjwa walikuwa wanasafiri kwenda hospitali ya Mkoa lakini kwa sasa imewapunguzia gharama kwa kupata huduma hapa hapa hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, huduma hii imesaidia sana na imefanikiwa kuwafikia watu wengi katika Wilaya yetu," amesema Dkt. Feisal.
Kwa upande wao, baadhi ya Wananchi waliopata huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho, Bi. Zainabu Thomas na Bi. Yasmin Seleman wameishukuru sana Serikali kwa huduma waliyopata. Wamesema walikuwa hawawezi kuona kabisa lakini kwa sasa wanaona. Walikuja hawawezi kutembea bila kushikwa mkono baada ya upasuaji wameweza kutembea wenyewe, hivyo basi wanashukuru sana kwa msaada huo wa matibabu.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa