Afisa Misitu wa Wilaya ya Ruangwa, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ndugu Solomon Masangya, amezindua rasmi Kamati ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA) ngazi ya Wilaya leo, Novemba 25, 2024. Uzinduzi huu ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mpango huu, ulioanzishwa mwaka 2016 na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, unalenga kutekeleza mikakati ya kitaifa na kimataifa ya kutokomeza ukatili kwa kushirikiana na sekta zote muhimu.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, Mpango Kazi wa Taifa wa Kudhibiti Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto umeundwa ili kuhakikisha wanawake na watoto wanaishi maisha ya heshima, usalama, na bila ukatili. Mpango huo unatekelezwa kwa njia za kisera, kisheria, kijamii, na kimuundo ili kuzuia aina zote za ukatili.
Miongoni mwa majukumu ya mpango huo ni kuandaa na kutekeleza kampeni za kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia, pamoja na kupambana na mila potofu kama ukeketaji na ndoa za utotoni. Vilevile, jamii inahamasishwa kubadili mitazamo na tabia zinazochochea ukatili kupitia programu za elimu kwa vijana na watu wazima.
Aidha, huduma za msaada kwa waathiriwa wa ukatili, zikiwemo huduma za afya, ushauri nasaha, na msaada wa kisheria, zimepewa kipaumbele. Hii ni pamoja na kuimarisha uwezo wa vyombo vya sheria, ikiwemo mahakama na polisi, ili kushughulikia kesi za ukatili kwa ufanisi zaidi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa