Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imeendesha mafunzo kwa watumishi wa ajira mpya 164 wa sekta mbalimbali, wakiwemo afya, utawala, kilimo na mifugo, na usafirishaji, ili kuwawezesha kuelewa taratibu za utumishi wa umma.
Mafunzo hayo yamefanyika Februari 12, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri kwa lengo la kuwaelimisha watumishi hao kuhusu kanuni, haki, na wajibu wao katika utumishi wa umma, sambamba na hilo, wamepewa elimu ya hifadhi ya jamii kupitia Mfuko wa PSSSF pamoja na usimamizi wa fedha kutoka kwa wawakilishi wa benki za CRDB na NMB.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Edger Komba ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utawala na usimamizi wa rasilimali watu, amesema Serikali inatarajia watumishi hao kuzingatia weledi, maadili na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
“Hii ni fursa muhimu kwenu kuelewa mazingira ya kazi na namna ya kutekeleza majukumu kwa kuzingatia taratibu za utumishi wa umma,” amesema Ndugu Komba.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa PSSSF Ndugu John Sombe ameongeza kuwa mfuko huo unahakikisha maslahi ya mtumishi wa umma yanazingatiwa hata baada ya kustaafu.
“Mnapaswa kufahamu haki zenu za mafao na michango yenu ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baada ya utumishi wenu,” amesema Ndugu Sombe.
Kwa upande wake, Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Denis Henry Temu, ambaye ni mtumishi mpya wa sekta ya afya, amesema mafunzo hayo yamempa mwanga kuhusu wajibu wake na namna ya kufuata taratibu sahihi.
“Nilikuwa sijui mambo mengi kuhusu taratibu za utumishi wa umma, lakini sasa nina uelewa mzuri wa haki na wajibu wangu,” amesema Temu.
Ikumbukwe, kupitia mafunzo haya Serikali inahakikisha kila mtumishi anakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu taratibu na kanuni za utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa