Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dr. Medadi Kalemani amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Lindi kutenga fedha zitakazofanya shughuli ya ‘wiring’ katika taasisi za umma katika msimu wa REA III.
Aliyasema hayo katika kijiji cha Chinongwe kilichopo katika Wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi alipokuwa anazindua mpango wa REA III.
Dr Kalemani aliwataka wakazi wa Kijiji cha Chinongwe waitumie fursa hiyo vizuri kwa kuweka umeme majumbani mwao, kwani wamepata bahati katika Wilaya zote zilizopo katika Mkoa wa Lindi wao wamepata nafasi ya kwanza ya kupata huduma hiyo.
“Umeme ni uchumi, umeme ni kila jambo tunakila sababu ya kuipongeza Serikali kwa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma nzuri za jamiii, hivyo msiishie kuweka umeme majumbani tu utumieni kufanya shughuli za kiuchumi”alisema Dr Kalemani.
Vilevile alimtaka Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Mkoa wa Lindi kufanya utaratibu wa kuanzisha madawati ya kuhudumia wateja wenye shida ya kuunganishiwa umeme katika vijiji ambavyo mradi unapita.
“Sitaki kusikia mwananchi anatembea kilometa 30 kwenda mjini kufuatilia suala la kuunganishiwa umeme nataka TANESCO ndiyo muwafuate wateja kwani mteja ni mfalme, mwiko mteja kumfuata TANESCO” alisema Dr Kalemani.
Pia alimtaka mkandarasi atakayekuwa anafanya ‘wiring’ katika makazi ya watu aidhinishwe na TANESCO wenyewe ili kuepuka vishoka na kuepuka suala la bei kutofautiana wakati zoezi hilo likiendelea.
“TANESCO chondechonde msiwawekee wananchi wetu bei kubwa ya kufanya ‘wiring’, bei iwe nafuu ili kila mwananchi aweze kupata huduma hiyo, tunataka kila mwananchi autumie umeme kuanzisha viwanda vidogovidogo”alisema Mh, Kalemani.
Naye Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Disima Namhanga alitoa pongezi kwa serikali kwa kuweza kusimamia na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma nzuri za kijamii.
“Serikali ya awamu ya tano inataka kila kijiji na vitongoji vyake umeme uweze kuwafikia wakazi wake na ndiyo maana umeme ni uchumi na umeme ni kila kitu wananchi watumie fursa hii vizuri”, alisema Namhanga.
Namhanga alisema vijiji 348 vilivyopo katika Mkoa wa Lindi vinatakiwa vipatiwe umeme, ila Wakandarasi wataanza na vijiji 175 ambavyo kazi yake itafanyika kwa wiki 24, wakimaliza hiyo wataendelea na vijiji 173 vitakavyobaki.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa