Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, ameongoza kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kilichofanyika leo Aprili 16, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kwa lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ongezeko la dozi ya pili ya chanjo ya polio (IPV).
Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe kutoka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, viongozi wa dini, Kamati ya Usimamizi wa Huduma za Afya Wilaya (CHMT), wawakilishi wa jamii, pamoja na Timu ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT). Wajumbe hao wamepatiwa elimu kuhusu utekelezaji wa utoaji wa chanjo, ili kuhakikisha kuwa jamii inafikiwa na ujumbe huo muhimu.
Aidha, utoaji wa dozi ya pili ya chanjo ya sindano ya polio (IPV) utafanyika kuanzia Mei 2025 kwa watoto wa umri wa miezi 9. Dozi ya kwanza ya chanjo hiyo hutolewa katika wiki ya 14, hivyo ongezeko hili linaongeza ufanisi wa kinga dhidi ya ugonjwa wa kupooza (poliomyelitis).
Vilevile, chanjo hiyo itaendelea kutolewa kupitia utaratibu wa kawaida wa utoaji wa chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na huduma za Mkoba, na imethibitishwa kuwa salama na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na kuidhinishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) chini ya Wizara ya Afya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha afya za watoto.
“Ongezeko hili la dozi ya pili ya chanjo ya polio ni hatua muhimu ya kulinda afya za watoto wetu dhidi ya ugonjwa hatari wa kupooza, Serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kila mtoto anayestahili anapata chanjo hii muhimu,” amesema Mhe. Ngoma.
Mbali na hayo, Serikali ya Wilaya ya Ruangwa imeendelea kusisitiza ushirikiano wa karibu kati ya jamii na wataalamu wa afya katika kuhakikisha watoto wote wanaostahili wanapatiwa chanjo hiyo, ili kujenga jamii yenye afya bora na kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa