Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, amemtaka mkandarasi kutoka kampuni ya JANIX CONSTRUCTION CO. LTD ya Iringa, anayetekeleza mradi wa uchimbaji wa kisima cha umwagiliaji katika Kijiji cha Nkowe, kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaohitajika kulingana na masharti ya mkataba. Ameyasema hayo leo, tarehe 06 Februari 2025, katika hafla ya kukabidhi mradi rasmi kwa mkandarasi ili kuanza utekelezaji.
Mhe. Ngoma amesema kuwa mradi huu ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa mazao, kuboresha kipato cha wakulima, na kuimarisha usalama wa chakula katika eneo la Nkowe na maeneo jirani. Hivyo, amesisitiza kuwa ni lazima mkandarasi kuhakikisha kazi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kuzingatia muda na viwango vya ubora vilivyokubaliwa.
Mradi huu unahusisha uchimbaji wa visima tisa (9) kwa awamu hii, ambapo visima vinne (4)vitachimbwa katika Halmashauri za Ruangwa, Mtama, Manispaa ya Lindi, na Kilwa, na visima vitano (5) vikichimbwa Mtwara. Utekelezaji wa mradi huu ulitangazwa kupitia zabuni, ambapo kampuni ya JANIX CONSTRUCTION CO. LTD ilishinda kandarasi kwa gharama ya TZS 408,870,000.00 (pamoja na VAT).
Meneja wa Mradi, Eng. Shamili Karama, ambaye ni Mhandisi Umwagiliaji wa Mkoa wa Lindi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, amesema kuwa atahakikisha mradi unakamilika kwa ufanisi na kwa wakati kama unavyotakiwa, ili kuwawezesha wakulima kunufaika na rasilimali za maji kwa kilimo cha umwagiliaji.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa