Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Hassan Ngoma ameongoza hafla ya uzinduzi wa uwanja wa michezo wa Ruangwa Veterans Sports Club uliopo Kilimahewa wilayani Ruangwa uwanja huo una ukubwa wa ekari 2.79 na uzinduzi wake umefanyika leo Juni 21 2025 kwa lengo la kuendeleza michezo na kukuza vipaji kwa vijana.
Ujenzi wa uwanja huo umegharimu jumla ya shilingi milioni 6.57 ambapo kati ya hizo milioni 5 zimetokana na michango ya wanachama wa klabu hiyo na zaidi ya milioni 1.5 zimepatikana kupitia nguvu kazi ya kujitolea. Miongoni mwa shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na kusafisha eneo, kutengeneza ‘pitch’, kupanda nyasi, kuweka magoli na kuvuta maji kwa matumizi ya uwanja.
Aidha, akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Ngoma amepongeza jitihada za wanachama wa timu hiyo kwa uzalendo, mshikamano na kujitoa kwa vitendo akibainisha kuwa jamii ya Ruangwa inahitaji taasisi kama hizi zinazochangia maendeleo kupitia michezo. Amesisitiza kuwa uwanja huo ni rasilimali ya pamoja inayopaswa kutunzwa na kuendelezwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. “Uwanja huu si kwa ajili ya Veterans pekee bali ni kwa jamii nzima Tutashirikiana nanyi kuhakikisha unaboreshwa zaidi,” amesema Mhe. Ngoma.
Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa klabu hiyo Ndugu Ramadhan Matola ameeleza kuwa Ruangwa Veterans Sports Club ilianzishwa mwaka 2020 ikiwa na wanachama 18 na hadi sasa ina wanachama hai 42 wakiwemo wanaume 39 na wanawake 3. Amefafanua kuwa maendeleo yaliyopatikana ni matokeo ya mshikamano wa wanachama na usaidizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
Hata hivyo, pamoja na hatua zilizofikiwa changamoto ya ukosefu wa uzio imeelezwa kuwa kikwazo kikubwa kwani uwanja umekuwa ukiingiliwa na mifugo hali inayosababisha uharibifu wa miundombinu. Sambamba na hilo, upungufu wa vifaa vya michezo na ukosefu wa udhamini umeendelea kudhoofisha kasi ya maendeleo ya klabu hiyo.
Kwa ujumla, viongozi wa timu wametoa wito kwa Serikali, wadau wa michezo na wafadhili binafsi kuunga mkono juhudi za wanachama kwa kusaidia ujenzi wa uzio utoaji wa vifaa na uwezeshaji wa programu za kukuza vipaji wilayani Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa