Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, leo Novemba 22, amefunga rasmi mafunzo ya Jeshi la Akiba katika kijiji cha Namkatila, Kata ya Matambarale, mafunzo hayo, ambayo yamehitimishwa kwa sherehe maalum, yamewezesha askari zaidi ya 100 kuhitimu kwa mafanikio makubwa, yakiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama wa wananchi na maendeleo ya Wilaya ya Ruangwa.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mhe. Ngoma amesema kijiji cha Namkatila kimefanya kazi ya kipekee katika maandalizi na utekelezaji wa programu hiyo, amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanaimarisha msingi wa maendeleo endelevu kwa Wilaya ya Ruangwa, huku akielezea kufurahishwa na kiwango cha nidhamu na ukakamavu ulioonyeshwa na wahitimu.
“Mmefunika, haijawahi kutokea,” amesema, akiwapongeza wakufunzi na wananchi kwa kushirikiana kikamilifu kufanikisha mpango huo.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea washiriki ujuzi muhimu wa kijeshi kama ujanja wa porini, matumizi ya silaha, usomaji wa ramani, na huduma ya kwanza. Vilevile, wahitimu walijifunza ujasiriamali, jambo ambalo Mhe. Ngoma amesema linachangia kuongeza ustawi wa kiuchumi kwa jamii, sambamba na kudumisha usalama wa eneo hilo.
“Mkawe watiifu na wazalendo kwa nchi yenu. Mafunzo haya ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa. Hakikisheni mnatii sheria, kanuni, na taratibu, na msitumie mafunzo haya vibaya kwa wananchi,” amesema, akiwahimiza wahitimu kutumia stadi walizopata kuleta manufaa kwa jamii yao.
Aidha, amewataka wananchi wa Ruangwa kushirikiana na vijana hawa waliopitia mafunzo ya Jeshi la Akiba kwa lengo la kuimarisha mshikamano na usalama. Mhe. Ngoma amesisitiza kuwa ukakamavu walionyesha wahitimu unapaswa kuwa chachu ya maendeleo na ustawi wa Wilaya nzima.
Ikumbukwe, Sherehe hizo zimeonesha mshikamano mkubwa wa jamii na mafanikio makubwa ya mafunzo hayo, ambayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha amani na usalama kama nyenzo ya maendeleo. Wahitimu wamesifiwa kwa ustahimilivu na juhudi zao, huku wakihimizwa kutumia ujuzi wao kwa njia chanya na yenye tija kwa Taifa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa