Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Hashim Mgandilwa amewataka watumishi sekta ya elimu hasa wanaosimamia miradi ya elimu katika kata na vijiji waliokwenda likizo, likizo zao zisitishwe na warudi Kwa ajili ya kusimamia vyumba vya madarasa, madawati, viti na meza katika shule zilizopo katika kata na vijiji vyao.
Amesema hayo wakati wa kikao na watendaji wa kata, vijiji na waratibu elimu kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kilichofanyika tarehe 24/12/2020 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya
“Hamkupaswa kwenda likizo kabisa kwani agizo la Waziri Mkuu lipo wazi na kwa kwenda likizo ina maana ya kukaidi maagizo na maelekezo ya viongozi wakuu wa serikali” amesema Mgandilwa.
Pia alisema ni wajibu wa kila Mtendaji wa vijiji kuitisha vikao vya ndani na mikutano mikuu ya hadhara Kwa kushirikiana na wenyeviti wa serikali za vijiji ili kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi kutimiza wajibu wao katika kufanya shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Ndg. Frank Fabian Chonya amewataka watendaji hao kuacha kuishi kwa mazoea na kufuata maagizo yanayotolewa na viongozi wakuu.
“Acheni kuwajibika kwa mazoea siwezi kuwa naagiza alafu nyie hamtekelezi maagizo yangu, tuache hizi tabia tuwajibike tutekeleze maagizo ya viongozi” amesema Chonya
Mkurugenzi aliwataka waratibu elimu kata kusimamia miradi ya elimu katika maeneo yao na na kuwataka kuibua miradi na ile ambayo haijaisha taarifa zake zipelekwe kwake kwa maandishi. Alisisitiza kukamilishwa Kwa miradi yote bila kujali ilianza lini.
Naye Mwanasheria wa Halmashauri Albert Mwombeki amewataka watumishi ambao wana kusanya fedha za serikali kwa kutumia mashine za kielektroniki kukusanyia mapato na kuacha kujikopesha fedha za serikali kwani ni kosa kubwa ambalo halivumiliki. Aliendelea kusema akigundulika mkusanya mapato ametumia fedha alizokusanya atambue kuwa mkono wa serikali utamkuta popote alipo. Aliwaasa watendaji hao kuwasilisha fedha benki kila wanapokusanya na si kukaa nazo au kujikopesha.
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa