Afisa Uandikishaji Jimbo la Ruangwa, Ndugu Frank Fabian Chonya, amewataka Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kufanya kazi kwa weledi na uadilifu katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili, akisisitiza kuwa Serikali imewaamini kutokana na uwezo na ujuzi walionao.
Chonya ameyasema hayo leo, Mei 14, 2025, wakati akifungua rasmi mafunzo ya Uboreshaji wa Daftari hilo awamu ya pili utakaoanza tarehe 16 Mei, 2025 hadi 22 Mei, 2025, mafunzo hayo yamefanyika katika bwalo la Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruangwa, yakihusisha Maafisa Waandikishaji kutoka kata zote za Wilaya ya Ruangwa.
Aidha, amesisitiza kuwa uteuzi wa maafisa hao si jambo la kawaida bali ni dhamana ya kitaifa inayopaswa kutekelezwa kwa bidii na uadilifu wa hali ya juu.
“Ni heshima kubwa kuaminiwa na kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kumbukeni hii ni dhamana ya kitaifa, zingatieni maadili na mwongozo wa Tume.” amesema Chonya.
Pamoja na hayo, amewakumbusha washiriki kuhakikisha wanashirikiana kikamilifu na Maafisa waandikishaji wa ngazi ya Kata na kuzingatia maadili ya kazi ili kuhakikisha kila hatua ya uandikishaji inafanyika kwa mujibu wa mwongozo wa Tume. Amesisitiza kuwa ushirikiano na uwajibikaji ni nguzo muhimu katika kufanikisha zoezi hilo.
Kwa upande mwingine, ameeleza kuwa ni muhimu kwa vyama vya siasa kupeleka mawakala wao katika vituo vya uandikishaji ili kuongeza uwazi na uaminifu wa mchakato huo, ingawa aliwakumbusha kuwa mawakala hao hawapaswi kuingilia majukumu ya maafisa waandikishaji. Ameonya kuwa nidhamu itazingatiwa kwa pande zote.
Zoezi hilo la kitaifa linatarajiwa kusaidia kuweka kumbukumbu sahihi ya wapiga kura na kuweka mazingira bora kwa ajili ya uchaguzi wa haki, huru na unaokubalika kwa pande zote, sambamba na kuimarisha demokrasia nchini.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa