Kinara wa Mfumo wa Watumishi Portal Mkoa wa Lindi, Ndugu Mohamed Chilemba, ametoa mafunzo kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule, na Maafisa Elimu Kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa leo 02 Decemba 2024 katika bwalo la shule ya sekondari Ruangwa, ili kuwaimarisha katika matumizi ya Mfumo wa Watumishi Portal, hatua inayolenga kuboresha utendaji kazi na ufanisi katika sekta ya elimu.
Mafunzo hayo yamejikita katika sehemu ya e-Utendaji (Watumishi), hususan kipengele cha Tathmini ya Utendaji wa Mtumishi (Assessment), ambacho ni muhimu kuelekea zoezi la tathmini ya utendaji kwa watumishi wa kada ya ualimu linalotarajiwa kuanza hivi karibuni. Aidha, Ndugu Chilemba amewahimiza washiriki kuhakikisha wanatumia mfumo huo kikamilifu ili kuondoa dosari za kiutendaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii.
Hata hivyo, katika mafunzo hayo, Ndugu Chilemba ameweka msisitizo maalum juu ya kuwasilisha changamoto zinazojitokeza mapema kwa ajili ya kupata suluhisho. Amesema kuwa mfumo huu ni nyenzo muhimu ya kuboresha uwajibikaji na uwazi kwa watumishi wa umma, na mafanikio yake yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya watumishi na viongozi wao.
Vile vile, amewapongeza Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule, na Maafisa Elimu Kata kwa kushiriki katika mafunzo hayo, akibainisha kuwa ari yao inaonesha dhamira ya dhati ya kuboresha elimu katika Wilaya ya Ruangwa, huku akisisitiza kwamba mfumo huo utaimarisha usimamizi wa watumishi wa umma, hasa katika kufuatilia na kutathmini maendeleo ya kiutendaji ya kila mtumishi.
Washiriki wa mafunzo hayo wamepongeza juhudi za Kinara huyo, wakisema kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kupata uelewa wa kina kuhusu matumizi ya mfumo huo, wameeleza kuwa mfumo wa Watumishi Portal ni zana muhimu katika utumishi wa umma.
Ikumbukwe, Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha mifumo ya kidijitali kwa watumishi wa umma, kwani yanachangia kuhakikisha kuwa watumishi anapimwa utendaji kazi wao kwa wakati, kwa uwazi, na kwa viwango vinavyostahili ili kuchangia maendeleo ya taifa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa