Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeendesha semina ya kipekee ya uwekezaji kwenye masoko ya dhamana za Serikali, ikilenga kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu fursa na umuhimu wa masoko hayo kwa uchumi wa Taifa, semina hiyo imefanyika leo, Septemba 19, 2024, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa.
Mafunzo hayo, yameongozwa na Simon Kessy, Meneja Msaidizi wa Fedha na Utawala kutoka BOT, huku yakiwaleta pamoja watumishi wa umma, wastaafu, na wadau wengine muhimu ili kuwapa maarifa ya namna wanavyoweza kushiriki katika masoko ya dhamana za Serikali, yenye faida kwa uwekezaji wa muda mrefu.
Aidha, katika maelezo yake Kessy amesisitiza kuwa uwekezaji kwenye dhamana za Serikali sio tu njia salama ya kuweka akiba, bali pia ni njia nzuri ya kuongeza mapato na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Amefafanua jinsi wananchi wanavyoweza kushiriki kwenye masoko hayo kupitia mifumo rasmi kama Benki Kuu na taasisi za fedha zilizoidhinishwa.
Kwa upande wao, washiriki wa semina hiyo wameipokea vyema, wakionesha shauku kubwa ya kujifunza na kushiriki katika uwekezaji huo. Akizungumza katika mafunzo hayo Mzee Mohamed Issa amesema “wastaafu na watumishi wa umma wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kunufaika na fursa kama hizi, ambazo awali zilikuwa hazijulikani kwa wengi, japo mimi ni moja ya washiriki wa hisa za mwanzo kabisa wakati bado zikiitwa vipande, natumaini kwa kipindi hiki masoko haya yameboreshwa zaidi kuliko kipindi tunaanza”. Amesema Mzee Issa
Tangu zamani, elimu juu ya masoko ya dhamana za Serikali imekuwa changamoto kwa wananchi wengi, hasa maeneo ya vijijini. Hata hivyo, juhudi za sasa za BOT zinaonesha matumaini mapya, huku lengo likiwa ni kuhakikisha watu wa kawaida wanashiriki katika uchumi wa nchi kupitia uwekezaji huu. Ili kufanikisha hili, serikali inapaswa kuendelea kutoa semina zaidi, kuongeza upatikanaji wa taarifa, na kuimarisha ushirikiano kati ya BOT na taasisi za kifedha ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa