Kampuni ya simu za mkononi Airtel Tanzania, kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na UNICEF, imekabidhi vifaa vya intaneti aina ya router kwa shule 23 za sekondari wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha elimu kidijitali nchini.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Agosti 20, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, yakihusisha shule mbalimbali zikiwemo Chienjere, Chinongwe, Chunyu, Hawa Mchopa, Kitandi, Mandawa, Ruangwa, Kassim Majaliwa, Likunja, Nkowe, Mnacho, Nambawala, Mbekenyera, Mbwemkuru, Narungombe, Michenga, Mandarawe, Liuguru, Lucas Maria, Namichiga, Mary Majaliwa, Ruangwa Wasichana pamoja na Samia Suluhu Hassan.
Kupitia vifaa hivyo, walimu na wanafunzi sasa watapata nafasi ya kufikia moja kwa moja maktaba mtandao ya TET na jukwaa la Shule Direct, hatua inayotarajiwa kuinua viwango vya ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Aidha, walimu wa TEHAMA na wakuu wa shule wamepatiwa mafunzo maalum ya matumizi ya vifaa hivyo kutoka kwa Mwalimu wa Airtel Smart Wasomi, Harrison Isdory, ili kuhakikisha vinatumika kwa ufanisi katika kuongeza uelewa wa wanafunzi.
Akizungumza katika tukio hilo, Meneja wa Airtel Mkoa wa Lindi, Salehe Saphy, alisema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wa elimu kuhakikisha kila mwanafunzi nchini anapata fursa ya kujifunza kwa njia ya kidijitali bila malipo.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Lindi, Mwl. Kurwa James, aliwataka walimu kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa tija na kulindwa ili viwe na manufaa ya muda mrefu kwa maendeleo ya elimu.
Naye, Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Ruangwa, Mwl. Ernest Haule, aliishukuru Airtel, TET na UNICEF kwa mchango huo, huku akibainisha kuwa hatua hiyo inaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha elimu nchini.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa